Nairobi, Machi 27, 2024 – Nyumbani katika mabara yote chakula kinachoharibika ni zaidi ya milo bilioni moja kwa siku katika mwaka wa 2022, huku watu milioni 783 wakiathiriwa na baa la njaa na theluthi moja ya wanadamu walikabiliwa na uhaba wa chakula. Uharibifu wa chakula unaendeleakuathiri vibaya uchumi duniani na kuzidisha mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, na uchafuzi. Haya ni matokeo muhimu ya ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) iliyochapishwa leo, tunapoelekea Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa.
Ripoti ya UNEP ya Data ya Uharibifu wa Chakula Mwaka wa 2024, iliyoandikwa na WRAP, inatoa makadirio sahihi zaidi ya kimataifa kuhusu uharibifu wa chakula wakati wa uuzaji na matumizi. Inatoa mwongozo kwa nchi kuhusu uboreshaji wa ukusanyaji wa data na kupendekeza mbinu bora za kuachacha na upimaji na kuanza kushughulikia uharibifu wa chakula.
Katika mwaka wa 2022 kulikuwa na tani bilioni 1.05 za taka za chakula zilizozalishwa (ikiwa ni pamoja na sehemu zisizoweza kuliwa), kiasi cha kilo 132 kwa kila mtu na karibu humsi moja ya chakula chote kinachofikia watumiaji. Kati ya jumla ya chakula chote kilichoharibika kataika mwaka wa 2022, asilimia 60 ilitokea nyumbani, huku huduma za chakula zikiwasilisha asilimia 28 na mahali kinapouzwa asilimia 12.
"Uharibifu wa chakula ni janga la kimataifa. Mamilioni ya watu watalala njaa leo ili hali chakula kinaharibiwa kote ulimwenguni," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Suala hili haliathiri tu maendeleo, ila athari za uharibifu huu usiohitajika zinagharimu mno tabianchi na mazingira. Habari njema ni kwamba tunajuwa kuwa iwapo nchi zitatoa kipaumbele kwa suala hili, zinaweza kupunguza uharibifu na utupaji wa chakula kwa kiwango kikubwa, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na hasara kwa uchumi, na kuimarisha hatua za kufikia malengo ya kimataifa."
Tangu mwaka wa 2021, kumekuwa na uimarishaji wa miundombinu ya data huku tafiti zaidi zikifuatilia uharibifu wa chakula. Kote duniani, kiwango cha data za nyumbani kiliongezeka takribani maradufu. Hata hivyo, nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati zinaendelea kutokuwa na mifumo ya kutosha ya kufuatilia hatua za kufikia Lengo la Maendeleo Endelevu la 12.3 la kupunguza kwa nusu uharibifu wa chakula kufikia mwaka wa 2030, hasa maeneo ya uuzaji na watoa huduma za chakula.
Ni nchi nne pekee za G20 (Australia, Japan, Uingereza, Marekani) na Muungano wa Ulaya ndizo zilizo na makadirio mwafaka ya uharibifu wa chakula ya kufuatilia hatua zitakazopigwa hadi mwaka wa 2030. Canada na Saudi Arabia zina makadirio mwafaka ya nyumbani, huku makadirio ya Brazili yakitarajiwa mwishoni mwa mwaka wa 2024. Katika muktadha huu, ripoti hii inatumika kama mwongozo wa vitendo kwa nchi kutumia kupima na kuripoti kuhusu uharibifu wa chakula mara kwa mara.
Takwimu zinathibitisha kwamba uharibifu wa chakula huathiri tu 'nchi tajiri', huku viwango vya uharibifu wa chakula nyumbani vikitofautiana katika viwango vya wastani vinavyozingatiwa katika nchi za kipato cha juu, cha juu kiasi, na cha kati cha chini kiasi kwa kilo 7 tu kwa kila mtu kwa mwaka. Wakati uo huo, nchi zilizo na joto zaidi zinaonekana kuzalisha taka nyingi zaidi za chakula kwa kila mtu nyumbani, kutokana na uwezekano wa matumizi ya juu ya vyakula kutoka shambani vyenye sehemu kubwa zisizoweza kuliwa na ukosefu wa jinsi ya kudumisha ubaridi.
Kwa mjibu wa data ya hivi karibuni, utupaji na uharibifu wa chakula huchangia kati ya asilimia 8 na 10 ya uzalishaji wa gesi ya ukaa (GHG) duniani - na uharibifu mkubwa wa bayoanuai kwa kuchukua sawa na karibu theluthi moja ya ardhi ya kilimo duniani. Shinikizo la utupaji na uharibifu wa chakula kwa uchumi duniani unakadiriwa kuwa takriban dola za Marekani trilioni 1.
Maeneo ya mijini yanatarajiwa kunufaika hasa kutokana na juhudi za kuimarisha upunguzaji wa uharibifu wa chakula na jinsi unavyofanywa. Maeneo ya vijijini kwa ujumla huharibu chakula kidogo, huku mabaki ya chakula yakielekezwa kwa wanyama wa nyumbani, mifugo, na utengenezaji wa mbolea nyumbani kama maelezo yanayoweza kutolewa.
Kufikia mwaka wa 2022, ni nchi 21 pekee ambazo zilikuwa zimejumuisha utupaji wa chakula na/au upunguzaji wa uharibifu wake katika mipango yake ya kitaifa ya tabianchi (NDCs). Mchakato wa kupitia upya NDCs katika mwaka wa 2025 unatoa fursa muhimu ya kuimarisha matarajio ya tabianchi kwa kujumuisha utupaji na uharibifu wa chakula. Ripoti hiyo pia inasisitiza dharura inahitajika kushughulikia uuharibifu wa chakula katika viwango vya mtu binafsi na vya kimfumo.
Misingi thabiti na vipimo vya kawaida vinahitajika ili nchi zionyeshe mabadiliko muda unaposonga. Kutokana na utekelezaji wa sera na ushirikiano, nchi kama vile Japan na Uingereza zinaonyesha kuwa mabadiliko kwa kiwango kikubwa yanawezekana, na upunguzaji wa asilimia 31 na 18 mtawalia.
"Kutokana na gharama kubwa kwa mazingira, jamii, na kwa uchumi wa kimataifa zinazosababishwa na uharibifu wa chakula, tunahitaji hatua zaidi zilizoratibiwa katika mabara na mifumo ya usambazaji. Tunaunga mkono UNEP katika kutoa wito kwa nchi zaidi za G20 kupima uharibifu wa chakula na kufanya kazi kufikia SDG12.3,” alisema Harriet Lamb, Mkurugenzi Mtendaji wa WRAP. "Hii ni muhimu ili kuhakikisha chakula kinaliwa na watu, na wala sio na madampo. Ushirikiano wa Sekta ya Umma na sekta Binafsi ni zana moja muhimu inayozalisha matunda kwa sasa, lakini unahitaji kupigwa jeki: iwe ni kutoka kwa wahisani, mashirika ya biashara, au ya kiserikali, wahusika ni sharti waunge mkono mipango inayoshughulikia athari kubwa inayotokana na unaribifu wa chakula kwa utoshelezaji wa chakula, kwa tabianchi, na kwa "mifuko yetu.”
UNEP inaendelea kufuatilia hatua zinazopigwa na nchi ili kupunguza kwa nusu uharibifu wa chakula kufikia mwaka wa 2030, huku msisitizo zaidi ukiwekwa kwa masuluhisho. Mbali na upimaji kuwe na kupunguza uharibifu. Suluhisho moja la aina hii ni hatua za kimfumo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs): Kuleta sekta ya umma, sekta ya kibinafsi na sekta zisizo za serikali kufanya kazi pamoja, kutambua vikwazo, kukuza masuluhisho pamoja, na kuendeleza hatua. Ufadhili mwafaka unaweza kuwezesha PPP kupunguza uharibifu wa chakula kutoka shambani hadi mezani, kupunguza uzalishaji wa GHGs na shinikizo kwa maji, huku tukishiriki mbinu bora zaidi na kuhimiza uvumbuzi ili kuwa na mabadiliko ya muda mrefu na ya jumla. PPPs kuhusu utupaji na uharibifu wa chakula zinaongezeka kote duniani, ikiwa ni pamoja na nchini Australia, Indonesia, Mexico, Afrika Kusini, na Uingereza ambako zimesaidia kupunguza zaidi ya robo ya uharibifu wa chakula wa nyumbani kwa kila mtu katika mwaka 2007-2018.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kuhusu WRAP
WRAP ni NGO ya kimataifa iliyo na makao yake nchini Uingereza. Ni mojawapo ya mashirika 5 ya ngazi ya juu zaidi yanayotoa misaada ya kimazingira nchini Uingereza na hushirikiana na serikali, wafanyabiashara na watu binafsi kuhakikisha kwamba malighafi duniani zinatumika kwa njia endelevu. Shirika lililoanzishwa mwaka wa 2000 nchini Uingereza, WRAP sasa hufanya kazi kote duniani na ni Mshirika wa Muungano wa Kimataifa wa Tuzo la Earthshot la Wakfu wa Royal.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa