Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Septemba, inalenga kuhamasisha na kuchukua hatua za kimataifa za kukabiliana na uchafuzi wa hewa, ambao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hivi majuzi aliuita "janga la kimataifa."
Vichafuzi vinavyopeperushwa hewani ni matishio makuu zaidi ya moja kwa moja kutoka kwa mazingira kwa afya katika nyakati zetu, huku asilimia 99 ya watu duniani wakivuta hewa isiyo salama. Kukumbana na uchafuzi wa hewa huongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano vya kukumbwa na viharusi, ugonjwa wa moyo na mapafu, saratani na magonjwa mengine, na kupelekea vifo vya mapema zaidi ya milioni 6.7 kwa mwaka.
Katika maadhimisho ya nne ya kila mwaka ya Siku ya Hewa Safi, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) liliketi chini na Martina Otto, mkuu wa sekretarieti ya Muungano wa Mazingira na Hewa Safi chini ya UNEP, ili kufahamu jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na janga la uchafuzi wa hewa.
Kwa nini Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu ni muhimu?
Martina Otto (MO): Karibu kila mtu huvuta hewa chafu. Lakini sisi sote hatuvuti hewa ileile - kutofautiana kwa viwango vya uchafuzi wa hewa mara nyingi hutokana na ukosefu mwingine wa usawa. Kukumbana na uchafuzi wa hewa kwa kiwango chochote unaweza kuwa na athari za kiafya ambazo hudhoofisha maisha na kugharamu mtu binafsi, jamii zetu na uchumi wetu.
Kama vile kupunguza uchafuzi wa hewa ni muhimu katika kuboresha afya ya binadamu, pia ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na wa bayoanuai, na uchafuzi na taka pamoja na kutusaidia kufikia Malengo kadhaa ya Maendeleo Endelevu.
Siku ya Hewa Safi huimarisha uelewa kuhusu athari mbaya za uchafuzi wa hewa na kuleta pamoja watafiti, mashirika ya biashara, serikali na watu binafsi kushughulikia masuala haya.
Je, ni nini umuhimu wa kaulimbiu ya mwaka huu ya Pamoja Kuwa na Hewa Safi?
MO: Tuna masuluhisho ya kukabiliana na tatizo la uchafuzi wa hewa lakini ili kuyatekeleza kwa kiwango kikubwa, sote tunahitaji kuja pamoja, kushirikiana na sekta mbalimbali na mamlaka mbalimbali za kisheria. Ingawa uchafuzi wa hewa huathiri kwa kiasi kikubwa maeneo yalio karibu na chanzo chake, unaweza pia kusafiri zaidi ya maelfu ya kilomita angani.
Hatuna ushawishi kuhusu jinsi upepo unavyovuma lakini tunaweza kushirikiana kutafuta masuluhisho kwa changamoto za kisheria na utekelezaji wake. Kwa mfano, uwekezaji unaweza kutumia mabaki ya kilimo kuwa rasilimali au nishati muhimu, na hivyo kupunguza uchomaji wake hadharani. Kwa kuwa tatizo linalovuka mipaka, kushughulikiauchafuzi wa hewa kwa njia bora kunamaanisha kutafuta masuluhisho ya kuvuka mipaka, kuwezesha ushirikiano kati ya miji na maeneo yanayoizunguka, na kuanzisha makubaliano ya kikanda na jukwaa la kimataifa ambalo linawezesha kubadilishana maarifa katika ngazi ya kikanda.
Ndio maana kaulimbiu ya mwaka huu inaangazia umuhimu wa ushirikiano thabiti, kuimarisha uwekezaji na kuwajibika pamoja. Tunahitaji hatua katika ngazi zote kutoka kwa washikadau wote katika sekta zote.
Baadhi ya vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa ni vipi?
MO: Ingawa uchafuzi wa hewa unaweza kutokana na vyanzo vya kiasili, kama vile milipuko ya volkeno na dhoruba za vumbi, idadi kubwa ya watu duniani huathiriwa na uchafuzi wa hewa unaosababishwa na binadamu. Vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa kutokana na binadamu ni pamoja na uzalishaji wa umeme, uchukuzii, viwanda, kuongeza joto na kupika majumbani, kilimo, na uchomaji taka. Nyingi kati ya vyanzo hivi pia huzalisha gesi ya ukaa, na baadhi ya vichafuzi hivi husababisha madhara maradufu, na kupelekea uchafuzi wa hewa na ongezeko la joto haraka.
Je, uchafuzi wa hewa unaathiri vipi afya ya binadamu?
MO: Uchafuzi wa hewa kwa ujumla ni tishio kuu kwa afya ya binadamu, lakini tunajali hasa athari za PM2.5. Hizi hazionekani kwa kutumia jicho la mwanadamu na ni ndogo mara 40 kuliko upana wa unywele wa binadamu. Kutokana na udogo wake, chembe hizi ndogo zinaweza kupenya ndani ya mapafu yetu, na kupelekea uvimbe, na pia zinaweza kupita hadi kwenye damu yetu na kudhuru moyo na ubongo wetu.
Uchafuzi wa mazingira una athari za kudumu - kama vile ugonjwa wa moyo, saratani, na kiharusi - na athari za muda mfupi, ikiwa ni pamoja na kuwashwawashwa kwa macho, pua na koo, kushindwa kupumua, kikohozi, na pumu.
Huwa tunaelezea athari za kiafya kupitia idadi ya vifo vya mapema. Lakini kiwango cha ubora wa maisha yetu ya kila siku huathiriwa pia. Uchafuzi wa hewa huathiri watu wa umri wowote ila kuna wale walio hatarini zaidi. Inaweza hata kuathiri ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
Tunaweza kufanya nini ili kuimarisha ubora wa hewa?
MO: Mikakati ya hewa safi inatofautiana kutegemea eneo husika. Hakuna suluhisho moja kwa hali zote; kuimarisha ubora wa hewa kunahitaji masuluhisho mengi katika sekta mbalimbali. Hata hivyo, sote tuna uwezo na lazima tuchukue hatua. Watu binafsi wanapaswa kufanya maamuzi yatakayokuza hewa safi. Mashirika ya biashara na viwanda wanaweza kutochafua kupitia michakato na bidhaa zao katika mifumo mizima ya utengenezaji na usambasaji wa bidhaa. Ni lazima pia kutoa kipaumbele hewa safi katika upangaji miji na sheria za serikali za mitaa na serikali kuu na utekelezaji wake.
Kuna vipengele vichache vya mara kwa mara kuhusiana na suala hili. Serikali zinaweza kuweka na kutekeleza viwango vya uchafuzi wa hewa na kufikia hatua muhimu zinazofuata zilizowekwa katika mwongozo wa mwaka wa 2021 wa Shirika la Afya Duniani. Wanapaswa pia kuimarisha uwezo wa kufuatilia na kutathmini ubora wa hewa. Mashirika ya biashara na viwanda wanaweza kuongeza ubora wa hewa kama sehemu ya shughuli zao za kuwajibikia jamii, kuripoti na kufuatilia uchafuzi wanaofanya, na kuendeleza kikamilifu programu za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.
Je, kuna jambo lolote ambalo mtu wa kawaida anaweza kufanya kuhusu uchafuzi wa hewa?
MO: Uchafuzi mwingi wa hewa ni wa kimuundo na umejikita katika michakato ya kiuchumi inayopatikana katika jamii za kisasa, kwa hivyo lazima tuanze na watu binafsi kuelimishwa kuhusu viwango vya uchafuzi wa hewa mahali wanapoishi na jinsi unavyowaathiri. Tunaweza pia kuamua kununua vitu visivyochafua mazingira na kubadilisha jinsi tunavyosafiri na kupika. Ni lazima pia tutoe wito wa mabadiliko ya kimfumo kutoka kwa mashirika ya biashara na serikali za mitaa na serikali kuu. Juhudi za mtu binafsi zinaweza kuonekana kuwa kidogo lakini tukizingatia idadi ya watu kwenye sayari yetu, ni muhimu. Lazima tushirikiane ili kuwa na hewa safi.
Kila mwaka, tarehe 7 Septemba, ulimwengu huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu. Siku hii inalenga kuhamasisha na kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za kuimarisha ubora wa hewa. Ni wito kwa jamii ya kimataifa kutafuta njia mpya za kufanya mambo, kupunguza kiwango cha uchafuzi wa hewa tunachosababisha, na kuhakikisha kwamba kila mtu, popote alipo anaweza kufurahia haki yake ya kuvuta hewa safi.