Nairobi, Julai 27, 2023 – Idadi jumla ya kesi za mabadiliko ya tabianchi mahakamani imeongezeka maradufu tangu mwaka wa 2017 kote duniani. Matokeo haya, yaliyochapishwa leo na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Kituo cha Sheria cha Mabadiliko ya Tabianchi cha Sabin katika Chuo Kikuu cha Columbia, inaonyesha kuwa kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaanza kuwa nguzo muhimu ya kupelekea kushughulikia mazingira na kuyapatia haki.
Ripoti ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Duniani: Uchanganuzi wa Hali Mwaka wa 2023 inatokana na uchanganuzi wa kesi zinazojikita kwa sheria, sera na sayansi ya mabadiliko ya tabianchii kufikia tarehe 31 Desemba mwaka wa 2022 na Hifadhidata ya Kituo cha Sheria cha Mabadiliko ya Tabianchi cha Sabin nchini Marekani na Hifadhidata ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Ulimwenguni. Inazinduliwa siku moja kabla ya maadhimisho ya kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya tamko la upatikanaji wa mazingira safi na bora kama haki ya binadamu wote.
"Sera za mazingira zingali nyuma sana kwa kuzingatia kile kinachohitajika ili kudhibiti viwango vya joto duniani visizidi nyuzijoto 1.5, huku matukio mabaya ya hali ya hewa na joto kali vikichemsha sayari yetu," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Watu wanazidi kugeukia mahakama ili kukabiliana na janga la mabadiliko ya taianchi, ili kuwajibisha serikali na sekta binafsi na kufanya kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa nguzo muhimu ya kushughulikia mazingira na kukuza haki ya mazingira."
Ripoti hii inatoa muhtasari wa kesi muhimu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, ikijumuisha mafanikio ya kihistoria (tazama kesi zilizochaguliwa hapo chini). Kadiri upeo na kiwango cha kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinapoongezeka mara kwa mara, mfumo wa kisheria wa jinsi ya kuzishughulikia unapanuka, na kuunda nyanja ya sheria inayozidi kufafanuliwa vyema.
Idadi jumla ya kesi za mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka zaidi ya maradufu tangu toleo la kwanza kwa kuongezeka kutoka 884 katika mwaka wa 2017 hadi 2,180 katika mwaka wa 2022. Huku Marekani ikiongoza kwa kesi, kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinakita mizizi kote duniani, huku takriban asilimia 17 ya kesi zikiripotiwa katika nchi zinazoendelea, zikiwemo Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo (SIDS).
Hatua hizi za kisheria zilipelekwa kwa taasisi 65 kote duniani: katika mahakama ya kimataifa, kikanda na kitaifa, mabaraza ya hukumu, mashirika ya kimahakama, na taasisi nyingine zinazotoa hukumu ikijumuisha taratibu maalum za Umoja wa Mataifa na mahakama za upatanisho.
"Kuna pengo la kusikitisha linalozidi kuongezeka kati ya kiwango cha gesi ya ukaa kinachohitaji kupunguzwa duniani ili kufikia malengo ya joto duniani, na hatua ambazo serikali zinachukua kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Hii itasababisha watu wengi zaidi kukimbilia mahakamani. Ripoti hii itakuwa nyenzo muhimu sana kwa kila mtu ambaye anataka kupata matokeo bora zaidi kupitia majukwaa ya mahakama, na kuelewa ni nini kinachowezekana na kisichowezekana mahakamani,” alisema Michael Gerrard, Mkurugenzi wa Kitivo cha Kituo cha Sabin.
Ripoti hiyo inaonyesha jinsi sauti za makundi yaliyo hatarini zinavyosikika kote duniani: Kesi 34 zimeletwa na au kwa niaba ya watoto na vijana chini ya umri wa miaka 25, ikiwa ni pamoja na wasichana wenye umri wa miaka saba na tisa nchini Pakistan na India mtawalia, huku nchini Uswizi, walalamishi wanawasilisha kesi yao kwa kuzingatia athari tofauti za mabadiliko ya tabianchi kwa wanawake wazee.
Kesi maarufu zimepinga maamuzi ya serikali kuzingatia kutoendana kwa mradi na malengo ya Mkataba wa Paris au ahadi za kutozalisha gesi chafu za nchi. Kuongezeka kwa uhamasishaji kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika miaka ya hivi karibuni pia kumechochea hatua dhidi ya mashirika - hii ni pamoja na kesi zinazotaka kuwajibisha kampuni za fueli ya visukuku na wazalishaji wa gesi ya ukaa kwa madhara yao kwa mazingira.
Kwa mjibu wa ripoti hii, kesi zinazoendelea za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huwa kwa kikundi kimoja au zaidi kati ya makundi sita ya kesi: 1) kesi zinazotegemea haki za binadamu zilizoainishwa katika sheria za kimataifa na katiba za kitaifa; 2) shinikizo kwa mataifa yasiotekeleza sheria na sera zinazohusiana na mazingira; 3) walalamishi kutafuta kudumisha mafuta ya visukuku chini ya ardhi; 4) kupigania ufichuzi zaidi kuhusu mazingira na kukomesha kijifanya kujali sana; 5) kuwajibisha mashirika kushughulikia madhara kwa mazingira; 6) na madai yanayolalamikia kushindwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti hiyo inaonyesha jinsi mahakama zinavyopata uhusiano thabiti wa haki za binadamu na mabadiliko ya tabianchi. Hii inapelekea ulinzi mkubwa kwa makundi yaliyo hatarini zaidi katika jamii, pamoja na kuongezeka kwa uwajibikaji, uwazi na haki, kulazimisha serikali na mashirika kutekeleza malengo kapambe zaidi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kushughulikia hali.
Katika siku zijazo, ripoti inakadria kutakuwa na ongezeko la idadi ya kesi zinazohusiana na uhamiaji kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kesi zitakazoletwa na Watu wa Kiasili, jamii za wenyeji na watu wengine wanaoathiriwa kwa njia tofauti na mabadiliko tabianchi, na kesi zinazoshughulikia uwajibikiaji wa matukio mabaya ya hali ya hewa. Ripoti hiyo pia inatazamia changamoto za kutumia sayansi inayohusiana na mazingira pamoja na kuongezeka kwa kesi za "upinzani" dhidi ya walalamishi kwa lengo la kuvunja kanuni zinazokuza ushughulikiaji wa mazingira.
Kesi muhimu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na masuala yanayoangaziwa katika ripoti hii inajumuisha:
- Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema kwa mara ya kwanza kwamba nchi imekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu kupitia kutoweka sera na kutochukua hatua za kushughulikia mazingira, na kupata serikali ya Australia ilikiuka wajibu wake wa haki za binadamu kwa wakazi wa visiwa vya Torres Strait;
- Mahakama ya Juu zaidi ya Brazili ikishikilia kuwa Mkataba wa Paris ni mkataba wa haki za binadamu, ambao unafurahia hadhi ya "kimataifa";
- Mahakama ya Uholanzi iliamurisha kampuni ya mafuta na gesi ya Shell kutii Mkataba wa Paris na kupunguza uzalishaji wake wa gesi ya kabondiksidi kwa asilimia 45 kutoka kwa viwango vya mwaka wa 2019 kufikia mwaka wa 2030. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama kupata kampuni binafsi kuwa na wajibu wa kutekeleza Mkataba wa Paris.
- Mahakama ya Ujerumani ilifutilia mbali baadhi ya sehemu za Sheria za Shirikisho la Kulinda Hali ya Hewa kwa kutoendana na haki za kuishi na afya;
- Mahakama ya Paris ilishikilia kuwa kutochukua hatua za kushughulikia mazingira nchini Ufaransa na kushindwa kutimiza malengo yake ya bajeti ya gesi ya ukaa kumepelekea uharibifu wa ekolojia uhaouhusiana na mazingira;
- Mahakama ya Uingereza iligundua kuwa serikali ilikuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria chini ya Sheria yake ya Mabadiliko ya Tabianchi ya mwaka wa 2008 wakati wa kuidhinisha mkakati wake wa kutozalisha hewa chafu;
- Juhudi za kupata maoni ya ushauri kuhusu mabadiliko ya tabianchi kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Baraza ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari zinaanzishwa na kuendeshwa na Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Media, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa