Credit: Science Photo Library via AFP
19 Jun 2024 Tukio Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Jinsi mashirika yanayotumia sera ya sayansi yanavyopelekea masuluhisho kwa majanga ya sayari

Credit: Science Photo Library via AFP

Katika Mkutano wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 2022, Nchi Wanachama 190 zilikubali kuanzisha  taasisi mpya ambayo itatoa kwa watungasera habari thabiti na huru kuhusu kemikali, taka na uchafuzi wa mazingira.  Jopo jipya la sera ya sayansi  – linalotarajiwa kuanza kufanya kazi mapema kama mwaka wa 2025 – na litasaidia serikali, makampuni, wakulima na washikadau wengineo wengi kukabiliana na kile kinachojulikana kama janga linaloongezeka.

Tayari kuna majopo mawili ya sera za kimataifa za sayansi yanayoshughulikia masuala makuu ya mazingira. Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) hutathmini sayansi ya mabadiliko ya tabianchi na Jukwaa la Sera ya Sayansi kati ya Serikali la Huduma za Bayoanuai na za Mifumo ya Ekolojia (IPBES) yanazingatia sayansi ya bayoanuai na michango ya mazingira kwa watu. Yote mawili yametekeleza wajibu muhimu wa kuhakikisha hatua na maamuzi bora yanafanywa kwa kuzingatia taarifa, huku maelfu ya wanasayansi na wenye maarifa – kama vile Watu wa Kiasili - hufanya kazi pamoja ili kusambaza tafiti, ushahidi na sera za hivi karibuni za kupitia ripoti zinazokubaliwa na serikali kote ulimwenguni.  

Mwezi huu, kikundi kazi kilichoandaliwa na UNEP kilikusanyika katika jiji la Uswizi nchini Geneva ili kuamua muundo wa jopo jipya la sera ya sayansi, huku kikao cha kwanza cha baraza linalosimamia jopo hili kikitarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao. Tunapokielekea, hapa kuna maelezo ya kina kuhusu majopo ya sera ya sayansi na kwa nini ni muhimu. 

Jopo la sera ya sayansi ni nini? 

Majopo ya sera za sayansi yameundwa mahususi ili kuwapa wafanya maamuzi, ikiwa ni pamoja na serikali, maelezo wanayohitaji ili kuunda sera ya mazingira kutokana na hali halisi. Kazi ya mashirika ya sera za sayansi pia yanaweza kusaidia kuhamasisha kuhusu suala, na hata katika baadhi ya hali kuonya kuhusu majanga yanayoweza kutokea. Yanalenga kuimarisha hali ya sera ya sayansi – kwa kutafuta uwiano unaoweza kutekelezeka kati ya tathmini, na usambazaji na matumizi yake wakati wa kufanya maamuzi.  

Kwa nini ni muhimu? 

Mashirika ya sera ya sayansi ni chombo muhimu cha kupambana na changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchiuharibifu wa mazingira na bayoanuai, na uchafuzi na taka. Yanatathmini sayansi ya hivi karibuni ili kufikia makubaliano thabiti kuhusu nafasi ya sayansi na ushahidi.  

Mashirika ya sera ya sayansi yanasaidia ulimwengu kukuza masuluhisho yanayotokana na ushahidi yanayoweza kupimwa na yatakayopelekea kushughulikia vyema changamoto zinazotukabili sote za mazingira," anasema Sheila Aggarwal-Khan, Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda na Uchumi ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).    

"Kwa kujumuisha washikadau wote wanaohusika katika mfumo mzima wa suala fulani, majopo haya yanazingatia vipengele vyote vya kiufundi, kiuchumi, kimazingira, kiafya na kijamii vya tatizo fulani, na kuruhusu kuundwa kwa masuluhisho madhubuti."  

Nani hushiriki katika kazi ya mashirika ya sera ya sayansi?    

Wanasayansi mbalimbali, wawakilishi wa serikali na wahusika wengine, kama vile mashirika ya uraia, huchangia katika kazi ya mashirika haya. Matokeo yake, yanayokubaliwa na serikali wanachama, yanawakilisha ushahidi bora unaopatikana kuhusu mada mahususi. 

IPCC inaundwa na vikundi kazi vitatu na Kikosi Kazi cha Orodha ya Kitaifa ya Gesi ya Ukaa. Vikundi kazi vitatu hutathmini vipengele tofauti vya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na jinsi jamii zinavyoweza kukabiliana nayo na kuyashughulikia, pamoja na msingi halisi wa kisayansi wa mabadiliko ya tabianchi. IPBES hukusanya kikosi cha waandishi wa wataalamu wakuu duniani kuhusiana na mada mbalimbali - kama vile uhusiano kati ya uchavushaji na uzalishaji wa chakula, matumizi endelevu ya spishi za porini na spishi ngeni vamizi na jinsi ya kuzidhibiti.   

Maelfu ya wataalam kutoka kote duniani huchukua muda wao kutoa ripoti za tathmini za IPCC na IPBES.  Zinatumika kama msingi wa mazungumzo wakati wa michakato kama vile Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi linalofanyika kila mwaka chini ya Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), na Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuai linalofanyika kila baada ya miaka milili, chini ya Mkataba wa Uanuai wa Kibayolojia.  

Je, kumekuwa na mafanikio yepi? 

Ripoti ya kwanza na ya pili ya tathmini ya IPCC iliweka msingi wa makubaliano ya sasa ya tabianchi. Ripoti ya uzinduzi wa IPCC mwaka wa 1992 ilitekeleza wajibu katika kuundwa kwa UNFCCC na Kongamano la Tabianchi la Nchi Wanachama (COP), kongamano la kila mwaka la mazingira ambapo nchi hujadiliana kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ripoti ya tathmini ya ufuatiliaji wa IPCC  – na hasa sentensi "Uwiano wa ushahidi unapendekeza ushawishi unaoonekana wa binadamu juu ya mazingira duniani" - ilikuwa wakati muhimu wa hatua za kushughulikia mazingira. Ilizipatia nchi ushahidi wa kutosha kuanza kukubaliana na malengo ya kupunguza uzalishaji wake wa gesi ya ukaa. Hali hii ilipelekea Mkataba wa Kyoto katika mwaka wa 1997 na Mkataba wa Paris katika mwaka wa 2005. "Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 1988, kila Ripoti ya Tathmini ya IPCC imeacha athari za kudumu katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi," anasema Katibu wa IPCC Abdalah Mokssit.    

IPBES imetoa ripoti 11 tangu mwaka wa 2016, ikiwa ni pamoja na Ripoti ya Tathmini ya Kimataifa ya mwaka wa 2019 ambayo ilitahadharisha ulimwengu kuhusu upeo wa janga la bayoanuai duniani, na matokea yake kuwa spishi milioni 1 za mimea na wanyama sasa ziko hatarini kutoweka, nyingi ndani ya miongo kadhaa. Tathmini ya Spishi Vamizi ya IPBES ya mwaka wa 2023 ilifichua kwamba gharama za kila mwaka za kimataifa za uvamizi wa kibayolojia zinazidi Dola za Marekani bilioni 423 na kwamba spishi hizi zimechangia pakubwa katika asilimia 60 ya kutoweka kwa mimea na wanyama.   

"IPBES inahusu bayoanuai - maisha duniani katika vipengele vyake vyote muhimu. Inahusu michango na ubora wa maisha ya watu kutokana na mazingira,” anasema Katibu Mtendaji wa IPBES, Anne Larigauderie.  "Ni kuhusu sababu za kupotea kwa michango hii na, muhimu zaidi, IPBES pia inahusu maamuzi tunayofanya sisi sote." 

Kuwezesha sera ya sayansi kurekebisha tabaka la ozoni

Mashirika mengine na mikataba ya kimataifa ya mazingira huandaa vikundi vya wataalamu ili kuwezesha matumizi ya sera ya sayansi.  Mfano mmoja ni Jopo la Tathmini ya Teknolojia na Uchumi  lililoanzishwa mwaka wa 1990 na nchi zilizotia saini Mkataba wa Montreal, makubaliano ya kimataifa ambayo yanayodhibiti uzalishaji na matumizi ya vitu vinavyodhuru ozoni. Jopo hili hutoa maelezo kuhusu teknolojia mbadala ambazo zimewezesha kwa hakika kuacha matumizi ya vitu vinavyodhuru tabaka la ozoni, kama vile klorofluorokaboni (CFCs) na haloni.    

Wajibu wa mashirika ya sera ya sayansi unabadilikaje? 

Mashirika ya sera ya sayansi yataendelea kufanya kazi muhimu ambayo yamekuwa yakifanya, wataalam wanasema. Lakini yanaweza kutekeleza wajibu muhimu zaidi katika kutathmini hatua zilizopigwa kwenye mikataba muhimu ya kimataifa ya mazingira, kama vile Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai wa Kunming-Montreal. Mashirika ya sera ya sayansi pia yataendelea kusawazisha wajibu wake kati ya tathmini na usambazaji na utekelezaji wake katika kufanya maamuzi halisi ulimwenguni.  "Umuhimu wa sera unasalia kuwa kipaumbele kikuu cha IPCC ili wafanya maamuzi katika ngazi zote waweze kutumia ipasavyo sayansi bora inayopatikana na ya kisasa zaidi katika kuunda sera na vitendo vyao," Mokssit wa IPCC anasema. 

Kwa nini jopo jipya la sera ya sayansi kuhusu kemikali, taka na uchafuzi ni muhimu sana?   

 Uamuzi wa kuanzisha jopo hili utatoa kwa sehemu ya tatu ya changamoto za aina tatu duniani shirika lake la kisayansi. Uchafuzi unakadiriwa kusababisha vifo milioni 9 kwa mwaka kote duniani, huku vifo vinavyotokana na uchafuzi vikiongezeka kwa asilimia 66 kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita. Uchafuzi wa kemikali huongeza hatari ya vimelea sugu, hali iliyosababisha vifo vya moja kwa moja takribani milioni 1.3 na takribani vifo milioni 5 vinavyohusishwa nao katika mwaka wa 2019. Jopo jipya la sera ya sayansi litazisaidia nchi kutekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu kemikali, taka na uchafuzina kubainisha masuluhisho mwafaka kwa janga hili. 

 

Mfumo wa Kimataifa wa Kemikali ni mpango wa kina wa kuongoza nchi na washikadau kushughulikia kwa pamoja mzunguko wa kemikali, zikiwemo bidhaa na taka. Mfumo huo uliopitishwa mjini Bonn mwezi Septemba mwaka wa 2023, unajumuisha malengo matano ya kimkakati na shabaha 28 za usimamizi mzuri wa kemikali na taka, na maono ya mustakabali salama, wenye afya na endelevu.